Tunafuraha kushiriki  baadhi ya maoni tuliyopokea kutoka kwa wale wanaojihusisha na programu ya uwezeshwashaji wa kiroho wa vijana chipukizi katika maeneo ya vijijini  ya india

Mshiriki mwenye umri wa miaka 15, huelezea hali anayoiona katika jumuiya yake

Kitu kibaya kabisa kijijini ni ubaguzi wa kitabaka. Watu hupigana kwa sababu ya tabaka. Inaonekana kwangu kuwa  tunahitaji kuubadilisha ubaguzi huu wa kitabaka haraka sana. Tunapaswa kuishi pamoja kwa umoja. Hapa upo ugomvi kwa sababu hiyo.

…Kwa mfano, kama mtu ni wa tabaka la juu, na wewe ni wa tabaka la chini, watu wa tabaka la juu hawatakuruhusu kuingia katika nyumba yao. Lakini mimi sifikirii namna hii. Ninadhani wamekuja nyumbani kwangu, hivyo wanapaswa kukaa nami, kusali nami.  Kama tunavyosoma katika vitabu [vya vijana chipukizi], tunapawa kuishi kwa umoja ili kwamba ubaguzi wote ukomeshwe.

Na hivi ndivyo anavyouona mustakabali

Kikubwa nimejifunza kwamba katika  maisha yetu tunahitaji  tuchague jinsi tunavyotaka kutoa huduma—jinsi tunavyoweza kuwa wema. Tunahitaji kuvutafuta vipaji vyetu. Na ninafikiria nitakuwa mwalimu. Nitawafundisha watoto mambo haya. Ninajaribu kufanya hivi na sasa ninafundisha katika shule ya mama yangu.

Tukikumbuka hadithi kutoka “Kutembea Njia Nyoofu”, kijana mwenye miaka 14 hueleza

….Nilijifunza kutoka kwenye vitabu kwamba tunahitaji kuendelea kufanya juhudi. Kama tunajaribu kufanya jambo fulani na tunahangaika, tusiliache na kwenda moja kwa moja nyumbani. Tunapaswa kumaliza kazi, na ndipo tuweze kwenda nyumbani. Mithili ya kisa cha vyura—tunapaswa kufanya mambo kwa namna hiyo. Chura wa kwanza alishindwa na hakujaribu. Wa pili alijaribu kupikicha maziwa hadi siagi ilitokea. Kwa namna hii, tunapaswa pia kufanya juhudi… ninajaribu kufanya hivi kwenye masomo yangu—kila mara ninajitahidi kufanya juhudi na ninaendelea.

Kijana mwingine anarejelea kwenye “Pepo Nyanana za Uthibitisho”

Nilikuwa nacheza tu. Sikufanya kazi yoyote nyumbani na sikusikiliza ushauri wa mama na baba yangu. Pia sikupenda na sikuweke maanani kwenye masomo yangu. Nilipojiunga na darasa hili na nilipoona tajiriba ya Musonda na Rose na jinsi walivyosoma na wanavyoishi na mama na baba yao, moyo wangu ulivutika. Kwa kipindi kile nilipata umaizi kwamba kabla ya kusoma tunapaswa kuchagua lengo kwa ajili ya ni akina nani tunataka kuwa baada ya masomo.

Kijana mwenye miaka 16, ambaye kwa sasa anahudumia kama mhuishaji wa kundi la vijana chipukizi, huelezea hitaji la mabadiliko katika kijiji chake.

Katika kijiji changu watu wengi ni wacha Mungu wenye itikadi kali na watu wengi daima wako tayari kupigana. Hupigania vitu vidogo. Mtu mmoja hufikiri kwamba  kama kuna kipande kidogo cha ardhi hujichukulia na kuwa chake. Baba yangu alifungua kesi, baadaye tukaifuta kwa sababu yule mtu alikuwa mhalifu, na mwonevu, na hatukuwa na msaada. Kulikuwa mkutano ulioitishwa na  panchayat [ halmashauri ya kijiji]. Mkutanoni watu wengu walisema, “Ninyi ni wanyonge. Fungani kesi.” Kwa hiyo kesi ilifika mwisho, mambo yakawa sawa. Hatukufanya kitu chochote.  Niliridhika, nikamuachia Mungu. Hata hivyo jinsi vilivyo vitendo vya mtu ndivyo yatakavyokuwa matunda.…

Baada ya kuona hili, nilifikiri, “Je kama tusingekuwa namna hii? Ingekuwaje kama umoja na upendo vingetokea na kuhusu mawazo ya huduma yangetokea?” Ninafikiria kuvifanyia kazi vyote hivi kijijini na kuleta mabadiliko haya? Hivyo ninafanyia kazi hilo.

Hii hapa baadhi ya mipango yake

…baada ya kusoma ninahitaji kusaidia maendeleo ya kijiji. Ninataka kufanya jambo ili kijiji kiweze kuendelea kiasi na niweze kuisaidia familia yangu. Kwa hiyo sasa ninasoma, na kuhusu suala hili, nadhani nitawasomesha watoto wadogo, na nitatumia fedha kidogo nitakayopata kwa kazi hiyo kuisaidia kaya yangu na pia kukidhi mahitaji yangu mwenyewe. Ninawafundisha watoto, na kujisomesha mwenyewe.

Kijana mwenye miaka 17, pia anayetoa huduma kama mhuishaji, anaeleza kile alichofanya pale familia yake iliposhindwa kumsaidia kumaliza shule ya sekondari

Katika Pepo Nyanana za Uthibitisho, baba yake Chishimba aliachishwa kazi, na nilifikiria mfano wake na pia ule wa Godwin. Nilijaribu kufikiria aina ya kazi ambayo ningeweza kuifanya ambayo hakuna anayeifanya. Kwa hiyo nilipata kazi katika kiwanda cha uchapishaji na ninafanya kazi hapo takribani masaa 8 kila siku na ninapokea fedha ya kutosha kulipia masomo yangu.  Nilikwenda kuongea na mtu mmoja katika kijiji changu, nikamweleza shida yangu, naye akanipa kazi.  Sasa ninaamka saa 9 usiku, ninasoma kwa muda wa saa moja na nusu, halafu ninatengeneza staftahi yangu na ninakula. Saa 12 asubuhi ninakwenda kwenye darasa la ziada na kusoma hadi saa 5 asubuhi. Halafu baada ya kula,  ninakwenda kazini saa 5:30 asubuhi.

Mwanamke kijana mwenye umri wa miaka 21 na anayetoa huduma ya mhuishaji katika kijiji chake, pia anayewafundisha watoto masomo yao ya shuleni, anaeleza:

Hapa watoto husoma hadi darasa la 7, na baada ya hapo hawaendi popote kujiendeleza. Baadhi yao huacha shule hata kabla ya hapo. Nilianza kuwafunza baadhi ya watoto nyumbani kwangu. Mmoja wa mabinti alifanikiwa sana. Baada ya kufanya mtihani wake, aliweza kuingia katika shule ya kijiji jirani, na husafiri kwenda huko kila siku. Lolote litokealo, huendelea kuja hapa na ninamsaidia.

Mwanamke mwingine kijana mwenye umri wa miaka 20 anaeleza:

Nilitaka kuwa mhuishaji kwa sababu nilivutiwa na jinsi wahuishaji  wa kundi langu lililopita, walivyoeleza mambo, na jinsi nilivyojifunza. Ni jukumu la kila mmoja kushiriki na wengine kile wanachojifunza—hilo ndilo jambo bora. Mithili ya ua, linapochanua, husambaza manukato yake kila mahali, na kila mtu husema “Oh ua zuri sana hili, linanukia vizuri sana!” na sisi tunapaswa kuwa hivyo—lazima tuwafikie wengine.

Na, mwishowe, kijana mwenye umri wa miaka 18 alishiriki katika programu alipokuwa msichana, na ambaye kwa sasa anahudumu kama mhuishaji, anaeleza:

Hapo zamani, familia yangu ilizoea kusema kuwa wasichana hawapaswi kutoka nje. Lakini sasa wanasema, “Hapana. Mabinti na wavulana ni sawa. Binti atakwenda kusoma na kujifunza.”